Thursday, May 21, 2015

ADEBAYOR AENDELEA KULIA NA NDUGU ZAKE, ADAI ALITAKA KUJIUA KWA AJILI YAO.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Togo na klabu ya Tottenham Hotspurs, Emmanuel Adebayor amebainisha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook kuwa alifikiria kujiua kutokana na matatizo ya familia yake. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31, ambaye ameichezea Spurs mechi chache msimu huu, pia amedai kuwa alishikiwa kisu na kaka zake Kola na Peter aliyefariki Julai mwaka 2012. Adebayor amesema mara kadhaa amekuwa akitaka kukata tamaa na kumpigia dada yake kumuelezea nia yake hiyo. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa alipofikiria kwa makini akaona hata akifa hakuna atayejua taarifa hizo ndio maana ameamua kuziweka wazi ili watu wengine haswa wanaotoka katika familia za kiafrika waweze kujifunza kutoka kwake. Hii ni mara ya tatu Adebayor kutuma ujumbe katika facebook kuelezea jinsi walivyokorofishana na mama pamoja na ndugu zake, matatizo ambayo yanatishia kumaliza kipaji chake cha soka. Adebayor pia amedai siku akiwa amelala alishangaa kaka zake wawili kumuwekea kisu shingoni baada ya kukataa kumpa Kola mtaji wa kufanyia biashara ya magari wakati akiichezea Monaco. Adebayor ambaye pia amewahi kucheza katika klabu za Arsenal, Manchester City na Real Madrid, amekuwa akiichezea Spurs mwaka 2011, lakini amecheza mechi 10 pekee msimu huu na kufunga mabao mawili.

No comments:

Post a Comment