Tuesday, June 25, 2013

BALOTELLI NJE KOMBE LA MABARA.

DAKTARI wa timu ya taifa ya Italia, Enrico Castellacci ametangaza kuwa mshambuliaji nyota wa timu hiyo Mario Balotelli hatacheza tena mechi zilizobakia za Kombe la Shirikisho na anatakiwa kurudi nyumbani kwa ajili ya kupata matibabu ya msuli aliyopata. Taarifa hiyo ya daktari inashabihiana na ile iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Italia-FIGC iliyobainisha kuwa nyota huyo asingecheza mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo dhidi ya Hispania baada ya vipimo vya x-ray kuonyesha kuwa amechanika msuli wa paja lake la kushoto. FIGC walikuwa na mategemeo kuwa Balotelli angerejea katika mchezo wa fainali au wa kutafuta mshindi wa tatu lakini Castellacci alifuta matumaini ya nyota huyo kurejea tena kumalizia michuano hiyo kwa jinsi alivyoumia. Daktari huyo aliendelea kusema kuwa tayari ameshazungumza na kocha wa timu hiyo Cesar Prandelli na kukubaliana kumruhusu mchezaji wake kwenda katika klabu yake ya AC Milan ili kupata matibabu zaidi.

No comments:

Post a Comment