Friday, December 30, 2016

MICHO AACHA WANNE THE CRANES.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes Milutin Sredojevic Micho amewaacha wachezaji wanne akiwemo Ronald Mukiibi anayecheza soka la kulipwa nchini Ujerumani, kipa Ismail Watenga, Vitalis Tabu na Derrick Nsibambi. Micho amepunguza wachezaji kufuatia safari yao ya kuelekea nchini Tunisia leo kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika ambayo wanashiriki kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 39. Kocha huyo anatarajia kuwachuja wachezaji wengine watatu katika kikosi chake cha sasa cha wachezaji 26 ili abaki na kikosi cha wachezaji 23 wanaohitajika katika michuano hiyo. Akihojiwa Micho amesema walishaanza mazoezi yao toka Desemba 19 na mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Tunisia Januari 4 ndio utampatia kikosi chake kamili cha wachezaji 23 kabla ya kwenda kwenye kambi yao ya mwisho huko Dubai. Uganda itaanza kupambana na Ghana katika mchezo wao wa ufunguzi Januari 17 huko Port Gentil kabla ya kuivaa Misri na baadaye Mali katika mchezo wao wa mwisho wa kundi D.

No comments:

Post a Comment