Friday, December 23, 2016

MADRID WAPANGWA NA SEVILLA KOMBE LA MFALME.

KLABU ya Real Madrid imepangwa kucheza na Sevilla katika hatua ya timu 16 bora ya michuano ya Kombe la Mfalme. Mabingwa hao wa Ulaya na Dunia wanatarajiwa kuchuana na Sevilla iliyo chini ya Jorge Sampaoli ambao wanashikilia nafasi ya tatu katika La Liga, ikiwa kama marudiano baada ya kukutana katika Super Cup ya UEFA Agosti mwaka huu ambapo Madrid waliibuka kidedea. Ratiba hiyo inamaanisha Madrid na Sevilla watakutana katika mechi tatu katika kipindi kisichozidi siku 11 mwezi ujao, kufuatia mchezo wa ligi baina yao kuwa Januari 15. Mabingwa watetezi wa taji hilo Barcelona wao watakwaana na Athletic Bilbao ambao waliwafunga katika fainali ya msimu uliopita, wakati Atletico Madrid wao watapambana na Las Palmas. Valencia wao watapambana na Celta Vigo, Villarreal watacheza na Real Sociedad, Osasuna dhidi ya Eibar na Deportivo La Coruna watachuana na Alaves. Mechi za mkondo wa kwanza zinatarajiwa kuchezwa Januari 4 huku zile za marudiano zikichezwa Januari 11.

No comments:

Post a Comment