KIUNGO mahiri wa klabu ya Barcelona, Andres Iniesta anatarajiwa kuwa mchezaji anaelipwa zaidi katika timu hiyo baada ya Lionel Messi wakati atakapotia saini makubaliano ya mkataba mpya wiki ijayo. Habari hizi zitakuwa sio nzuri kwa klabu ya Real Madrid ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakimuwinda winga huyo wa kimataifa wa Hispania. Rais wa Barcelona, Sandro Rosell alitangaza Alhamisi kuwa Iniesta tayari amefikia makubaliano ya mdomo kuongeza mkataba wake mpaka 2018 ambapo anatarajiwa kukunja kitita cha paundi milioni 14 kwa msimu katika miaka minne ijayo ikiwa ni mara mbili ya kiasi anachopata sasa. Mpaka kufikia kipindi hicho nyota huyo atakuwa ametimiza miaka 34 na Rosell amebainisha kuwa anaweza kuongezwa mkataba zaidi kutokana na uwezo wake utakavyokuwa. Iniesta alianza kukitumikia kikosi cha kwanza cha Barcelona mwaka 2002 chini ya kocha Louis van Gaal ambapo mpaka sasa amecheza mechi 479 na kufunga mabao 48.
No comments:
Post a Comment