WAKATI vinara wa Bundesliga, Bayern Munich wakikabiliwa na mchezo wa fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia baadae leo, mahasimu wao katika ligi Borussia Dortmund na Bayer Leverkusen wataingia uwanjani ili kujaribu kupunguza pengo la alama baina yao. Bayern wanaongoza kwa tofauti ya alama saba katika msimamo wa ligi na wamekuwa tishio kunywakuwa taji hilo tena kama mahasimu wao hao hawatavuna alama wakati wakiwa nchini Morocco. Bayer Leverkusen ambao wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi watakuwa wageni wa Werder Bremen baadae leo huku wenyeji wakiwa wana kiu ya ushindi baada ya kuukosa katika mechi tano zilizopita. Kocha wa Bayer ambaye ni nyota wa zamani wa Liverpool, Sami Hyypia amesema hautakuwa mchezo rahisi kwao lakini wanataka kumaliza vyema kwa kuchukua alama zote tatu kabla ya mapumziko ya majira ya baridi. Borussia Dortmund wanaoshika nafasi ya tatu ambao wako nyuma ya Bayern kwa alama 12 na tano kwa Leverkusen, watakuwa wenyeji wa Hertha Berlin wakitafuta ushindi wao wa pili katika mechi tano za ligi walizocheza.
No comments:
Post a Comment