Monday, December 23, 2013

MPUTU AONDOKA TP MAZEMBE.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC, Tresor Mputu ameikacha klabu yake ya TP Mazembe na kuhamia kwa mabingwa wa soka nchini Angola timu ya Kabuscorp. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 alitangazwa mbele ya waandishi wa habari jijini Luanda kuwa amesaini mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya euro milioni mbili ambao utamuwezesha kukunja kitita cha euro 40,000 kwa mwezi. Mashabiki wa Mazembe wamekuwa wakipinga kuondoka kwa nyota huyo hatua ambayo imepelekea uongozi wa Mazembe kutoa taarifa ya kuwa kuondoka kwake hakutaathiri kiwango cha timu hiyo. Mputu ameitumikia Mazembe kwa miaka 10 akiisaidia timu hiyo kushinda taji la Klabu Bingwa barani Afrika mwaka 2009 na 2010 pamoja na kuweka historia ya kufika fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Duniani ambapo walifungwa na Inter Milan kwa mabao 3-0 mwaka 2010. Timu ya Kabuscorp ilitengeneza vichwa vya habari Januari mwaka jana wakati walipomsajili mshambuliaji nyota wa zamani wa Brazil Rivaldo aliyecheza soka nchini humo kwa msimu mmoja pekee.

No comments:

Post a Comment