Tuesday, May 28, 2013

BENITEZ KOCHA MPYA NAPOLI.

MENEJA wa zamani wa klabu za Inter Milan, Liverpool na Chelsea, Rafael Benitez anatarajia kurejea nchini Italia kuchukua mikoba ya kuinoa klabu ya Napoli. Rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis alithibitisha ujio wa kocha huyo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa twitter kwamba Benitez ndio atakuwa mbadala wa aliyekuwa kocha wa klabu hiyo Walter Mazzarri. Mazzarri alitema kibarua cha kuinoa klabu hiyo baada ya kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Juventus katika msimamo wa Ligi Kuu nchini Italia maarufu kama Serie A na kukata tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao. Mazzarri ameiongoza Napoli kwa kipindi cha miaka minne ambapo ameweza kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa mara mbili na kushinda Kombe la Italia mwaka jana ambapo katika barua yake ya kujiuzulu wadhifa huo alidai kuwa ameifikisha timu hiyo alipotaka. Benitez aliinoa Inter katika nusu ya kwanza ya msimu wa 2010-2011 baada ya kuchukua nafasi ya Mourinho lakini alimkasirisha mmiliki wa klabu hiyo baada ya kudai kuongezewa nguvu katika kikosi chake na kutimuliwa kabla ya kipindi cha Christmas mwaka 2011.

No comments:

Post a Comment