Tuesday, May 28, 2013
TAIFA STARS YAANZA KUJINOA ADDIS ABABA.
Taifa Stars imetua jijini Addis Ababa, Ethiopia leo (Mei 28 mwaka huu) alfajiri kwa ndege ya EgyptAir ambapo itaweka kambi ya wiki moja kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco (Lions of the Atlas) itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech. Stars iliyotua na kikosi cha wachezaji 21 imefikia hoteli ya Hilton, na imeanza mazoezi leo (Mei 28 mwaka huu) saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Addis. Kwa mujibu wa Kocha Kim Poulsen, Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa na vipindi (sessions) vinne vya mazoezi kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile). Mechi dhidi yan Sudan itachezwa Jumapili kuanzia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Addis. Sudan ambayo pia imeweka kambi yake Addis Ababa kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia ilicheza mechi yake ya kwanza jana (Mei 27 mwaka huu) dhidi ya wenyeji Ethiopia na kulala mabao 2-0. Wachezaji wanaounda Stars ni nahodha Juma Kaseja, nahodha msaidizi Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi. Kikosi hicho kinatarajiwa kuondoka Addis Ababa kwenda Marrakech alfajiri ya Juni 3 mwaka huu kwa ndege ya EgyptAir. Stars itatua siku hiyo hiyo Casabalanca na kuunganisha moja kwa moja kwenda Marrakech.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment