Monday, February 24, 2014

WENYEJI URUSI WAONGOZA KWA MEDALI MICHUANO YA OLIMPIKI YA BARIDI HUKO SOCHI.

MICHUANO ya 22 ya Olimpiki majira ya baridi imemalizika rasmi jana jijini Sochi baada ya siku 17 za mashindano hayo huku wenyeji Urusi wakiibuka kidedea kwa kuongoza kwa kuzoa medali. Zaidi ya wanariadha 2800 kutoka mataifa 88 walishiriki katika mashindano hayo yaliyojumuisha michezo 12 mpya ambapo Urusi walimaliza wakiwa wa kwanza katika jedwali la medali, wakiwa na medali 13 za dhahabu 11 za fedha na 9 za shaba. Norway ilimaliza katika nafasi ya pili baada ya kujizolea medali 11 za dhahabu 5 za fedha na 10 za shaba huku Canada wao wakiwa katika nafasi ya tatu kwa kuwa na medali 10 za dhahabu 10 za fedha na 5 za shaba. Akifunga mashindano hayo katika sherehe zilizochukua takribani dakika 130 rais wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa, IOC Thomas Bach aliitaka dunia kuitizama Urusi kwa mtazamo mpya kwani wamezidisha matarajio ya washiriki wengi walioshiriki mashindano hayo ya Sochi. Mara baada ya sherehe hizo wenyeji waliwakabidhi bendera ya olimpiki nchi ya Korea Kusini ambao ndio watakuwa wenyeji wa mashindano hayo 2018 katika mji wa Pyeongchang.

No comments:

Post a Comment