Friday, February 28, 2014

MAKALA: DROGBA KUTOA KITABU CHA VIKARAGOSI.

MSHAMBULIAJI nyota wa Ivory Coast alianza kutembea wakati ana miezi sita, akaondoka nyumbani akiwa na umri wa miaka mitano na kutumbukia katika dimbwi la mapenzi kwa mwanamke aliyekuja kuwa mke wake katika umri wa miaka 17.

Hizo ni baadhi ya dondoo za matukio ya maisha ya nyota huyo ambayo yatachapishwa rasmi katika mfumo wa vikaragosi nchini Ufaransa.

Pia kutakuwa na matoleo ya Uingereza ambapo Drogba bado anakubalika na mashabiki wa klabu yake ya zamani ya Chelsea, Brazil ambapo atakwenda kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia baadae mwaka huu na Uturuki ambapo sasa anacheza katika klabu ya Galatasaray.

Matukio hayo yatakuwa yakifuatilia safari ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 kutoka alipoanzia jijini Abidjan mpaka mafanikio aliyopata katika soka duniani.

Drogba alizaliwa Machi 11 mwaka 1978 ambapo alienda nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka mitano kuishi na mjomba wake Michel Goba ambaye naye alikuwa mcheza soka ambapo wazazi wake waliamini kuwa hatua itampa nafasi ya kuwa na maisha bora.

Ni mara chache nyota huyo amekuwa akizungumzia maisha magumu aliyopitia akiwa mdogo, muda mrefu aliotengana na wazazi wake na maisha ya kuzunguka kutokana na mjomba wake kubadilisha timu kila mara.

Wazazi wake waliungana naye Ufaransa wakati akiwa na miaka 13 na wakaweka makazi yao jijini Paris ambapo Drogba ndipo alipoanza safari yake ya soka katika timu ya Levallois SC.

Akihojiwa kuhusiana na kitabu hicho Drogba amesema kitakuwa na maelezo mengi juu ya mambo aliyopitia ili kuwaonyesha watoto kuwa wakipita mahali alipopita basi wanaweza kufanikisha malengo yao.

Sehemu ya mauzo ya kitabu hicho yatakwenda katika mfuko wa hisani uitwao Didier Drogba ambao husaidia mipango ya Afya na Elimu barani Afrika.

No comments:

Post a Comment