MENEJA wa klabu ya Juventus ya Italia, Antonio Conte anafikiri waamuzi wa soka wa Italia ndio bora duniani na wanastahili kuheshimiwa. Kauli ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 inakinzana na ile aliyotoa msimu uliopita wakati alipomshukia mwamuzi Marco Guida aliyechezesha mchezo kati ya Juventus na Genoa ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1. Hata hivyo, Conte amesisitiza kuwa amebadili mtazamo wake juu ya waamuzi wan chi hiyo. Akihojiwa Conte amesema hakupenda kilichotokea mwaka jana wakati alipotoa maneno makali kwa mwamuzi katika mchezo huo kwasababu kwa mawazo yake alidhani walistahili penati katika dakika za majeruhi lakini hawakupewa. Conte amesema alifanya makosa kufanya alivyofanya na tayari ameomba msamaha na kubadilisha mtazamo wake juu ya waamuzi kwani anadhani wanapaswa kuheshimiwa kwa kazi kubwa wanayofanya. Juventus inajiandaa na mchezo wake wa mkondo wa pili wa Europa League dhidi ya Trabzonspor utakaochezwa baadae leo huku wakiwa na akiba ya mabao 2-0 waliyopata katika mchezo wa kwanza waliocheza nyumbani.
No comments:
Post a Comment