Friday, February 21, 2014

TWIGA STARS, ZAMBIA SASA KUCHEZA FEB 28.

MECHI ya mkondo wa pili ya raundi ya kwanza kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake,AWC kati ya timu ya taifa ya Tanzania,Twiga Stars na Zambia inayojulikana kama Shepolopolo sasa itachezwa Februari 28 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam. Twiga Stars tayari ipo kambini kujiandaa kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni chini ya kocha Rogasian Kaijage huku wakifanya mazoezi yao kwenye Uwanja wa Karume ambao ni wa nyasi za bandia kama ulivyo ule wa Azam Complex. Shepolopolo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka na kama Twiga Stars wakifanikiwa kuiondoa Shepolopolo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Zimbabwe. Wakati huohuo Ligi Kuu ya Vodacom,VPL kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 19 kesho kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam, Bukoba, Morogoro, Tanga na Arusha. Kwa upande wa Dar es Salaam, Yanga watakuwa wageni wa Ruvu Shooting ya mkoa wa Pwani katika Uwanja wa Taifa, wakati huko Bukoba Kagera Sugar wataikaribisha Rhino Rangers ya Tabora katika Uwanja wa Kaitaba. Huko Morogoro katika Uwanja wa Manungu uliopo Turiani Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Ashanti United huku Coastal Union wakiwa na kibarua kigumu dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na maafande wa Oljoro JKT watakuwa nyumbani kupambana na Mgambo Shooting katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.


No comments:

Post a Comment