SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania, TFF na Symbion Power Tanzania Limited zimesaini makubaliano ambapo kampuni hiyo itasaidia kwenye maeneo matatu ya mpira wa miguu wa vijana. Katika taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura imedai kuwa makubaliano hayo yamefikiwa na kutiwa saini leo katika ofisi za shirikisho hilo mbele rais wake Jamal Malinzi na mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Peter Gathercoles.Maeneo ambayo Symbion itasaidia ni ujenzi wa vituo viwili vya kuendeleza vipaji vitakavyojengwa Kidongo Chekundu na Kinondoni mkoani Dar es Salaam, mashindano ya Taifa ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 12 yatakayofanyika mwaka huu na kuisaidia timu ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys. Kampuni hiyo imetoa jumla ya shilingo milioni 176 kwa ajili ya mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 12 na pia maandalizi ya Serengeti Boys kwa ajili ya mchezo wao wa mchujo kuwania tiketi ya michuano ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Afrika Kusini utakaochezwa Julai mwaka huu. Malinzi aliishukuru kampuni hiyo kwa kukubali kushirikiana na TFF katika mpira wa miguu wa vijana, lakini vilevile amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwani ndiye chachu ya kampuni hiyo kuamua kujishirikisha na mpira wa miguu wa vijana.
No comments:
Post a Comment