Sunday, August 25, 2013

DJOKOVIC, MURRAY WAMUHOFIA NADAL US OPEN.

MCHEZAJI nyota wa tenisi wa Serbia, Novak Djokovic amedai kuwa kiwango bora alichokuwa nacho Rafael Nadal katika kipindi hiki kinamfanya kuwa mgumu kufungika katika michuano ya wazi ya Marekani inayotarajiwa kuanza kesho. Nadal ambaye ni raia wa Hispania ameweka rekodi ya kushinda mechi 15 katika viwanja vigumu kwa mwaka huu na pia kushinda mataji ya Masters katika michuano ya Indian Wells, Montreal na Cincinnati. Djokovic alimsifu Nadal kwa kurejea katika kiwango chake baada ya kukaa nje ya uwanja kwa kipindi miezi saba akiuguza majeraha na kudai kuwa anadhani ndio mchezaji bora kwa mwaka huu na hilo halina ubishi. Mbali na Djokovic kumgwaya Nadal lakini pia Andy Murray wa Uingereza naye alionyesha kumhofia nyota huyo na kudai kuwa atakuwa moto wa kuotea mbali katika michuano hiyo itakayofanyika jijini New York.

No comments:

Post a Comment