Tuesday, August 27, 2013

MAJERUHI YAMSTAAFISHA DECO.

KIUNGO mahii wa kimataifa wa zamani wa Ureno, Deco ametangaza rasmi kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 35 baada ya kupata majeraha ya msuli kwa mara ya nne toka msimu wa Ligi Kuu nchini Brazil uanze Februari mwaka huu. Deco ambaye ni mzaliwa wa Brazil alikuwa akicheza katika klabu ya Fluminense kwa miaka zaidi ya mitatu na kuiwezesha timu hiyo yenye maskani yake jijini Rio de Janeiro kushinda mataji mawili ya ligi mwaka 2010 na 2012. Katika taarifa yake Deco alidai kuwa angependelea kuendelea kuisadia Fluminense zaidi lakini anaona mwili wake unakataa kutokana na umri alionao na kuwashukuru wote waliokuwa pamoja naye katika kipindi chote ambacho amekuwa akicheza soka. Kiungo huyo ambaye jina lake halisi anaitwa Anderson Luis de Souza anakabiliwa na tuhuma za kutumia madawa yaliyokatazwa michezoni mapema mwaka huu, kesi ambayo bado inashughulikiwa na mahakama ya juu wa michezo ya Brazil. Deco alianza soka lake katika klabu ya Corinthians ya Sao Paulo mwaka 1996 na baadae kwenda timu ya CSA de Alogoas kabla ya kutimkia Ureno ambako alicheza katika vilabu vya Alverca, Salgueiros na Porto ambako alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na Kombe la Mabara mwaka 2004.



Baada ya kutoka Porto alihamia Barcelona na kucheza kuanzia mwaka 2004 mpaka 2008 ambapo katika kipindi hicho alifanikiwa kushinda mataji mawili ya La Liga na Kombe la Mfalme mwaka 2005 na 2006 pamoja na taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2006.

No comments:

Post a Comment