Tuesday, August 27, 2013

WILLIAMS, NADAL WAPETA US OPEN.

MICHUANO ya wazi ya Marekani imeanza kutimua vumbi rasmi jijini New York jana kwa viwanja mbalimbali vya mji huo kuwaka moto. Bingwa mtetezi wa michuano hiyo kwa upande wa wanawake Serena Williams alianza kwa kishindo kwa kutinga mzunguko wa pili kirahisi baada ya kumgaragaza Francesca Schiavone wa Italia kwa 6-0 6-1. Williams aliyetumia muda wa saa moja pekee katika mchezo huo, amesema alikuwa akijitahidi kuwa mwangalifu kwasababu alikuwa akicheza na Schiavone ambaye ni bingwa wa zamani wa michuano ya wazi ya Ufaransa hivyo lolote lingeweza kutokea. Kwa upande wa wanaume Rafael Nadal wa Hispania ambaye aliwahi kuwa bingwa wa michuano hiyo mwaka 2010 naye alitinga mzunguko wa pili kwa kumgaragza Ryan Harrison wa Marekani kwa 6-4 6-2 6-2. Nadal ambaye alikosa kucheza michuano hiyo mwaka uliopita kutokana na kuwa majeruhi, mechi hiyo inakuwa ya kwanza kwake toka alipofungwa na Novak Djokovic katika fainali mwaka 2011.

No comments:

Post a Comment