Thursday, August 18, 2011
MECHI YA STARS NA ALGERIA KUCHEZWA MWANZA.
DAR ES SALAAM, Tanzania
MECHI ya mchujo ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) zitakazofanyika mwakani nchini Equatorial Guinea na Gabon katika ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Algeria (Desert Warriors) itachezwa Septemba 3 mwaka huu jijini Mwanza.
Awali tulipanga mechi hiyo ichezwe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Lakini uamuzi wa kuihamishia Mwanza umefanyika baada ya jana kupata barua kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ikitufahamisha kuwa Uwanja wa Taifa hautatumika tena kwa sasa. Kwa mujibu wa Wizara, uwanja huo utakuwa katika matengenezo baada ya kuharibika wakati wa michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika mwanzoni mwa mwezi uliopita.
YANGA, SIMBA NAZO KUATHIRIKA
Uamuzi huo wa uwanja kufungwa kwa ajili ya matengenezo pia umeziathiri klabu za Yanga na Simba ambazo zilikuwa zimekubaliwa timu zao zitumie kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom ambayo inaanza kutimua vumbi Agosti 20 mwaka huu.
Tayari leo (Agosti 18 mwaka huu) tumeziandikia rasmi klabu za Simba na Yanga kuzifahamisha kuhusu uamuzi huo wa Wizara, hivyo kuzitaka zitafute viwanja vingine kwa ajili ya mechi zao za ligi.
Hatua hiyo ya uwanja kufungwa, itailazimisha TFF ifanye mabadiliko kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuzingatia viwanja ambavyo klabu za Yanga na Simba zitakuwa zimeamua kuvitumia.
Mabadiliko hayo pia yataziathiri timu za African Lyon, Azam, JKT Ruvu, Moro United na Villa Squad ambazo licha ya kutumia Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam, zilipanga mechi zao za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga zichezwe Uwanja wa Taifa.
Kwa sasa msimamo wa wamiliki wa Uwanja wa Azam ni Yanga na Simba kutoutumia kwa vile uwezo wake wa kuchukua watazamaji ni mdogo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment