Wednesday, September 21, 2011

KIKOSI CHA STARS KITAKACHOPAMBANA NA MOROCCO KUTAJWA.

DAR ES SALAAM, Tanzania
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen anatarajia Septemba 26 mwaka huu kutaja wachezaji watakaoingia kambini kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Oktoba 9 mwaka huu jijini Casablanca.

Akizungumza Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura alisema kikosi hicho kinatarajiwa kujitupa kambini Septemba 28 kwa ajili ya kujjiwinda na mchezo huo ambapo inatarajiwa kuondoka Octoba 6 kwenda Casablanca.

Alisema mchezo huo ni wa mwisho wa hatua ya makundi wa kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazotarajiwa kufanyika kwa pamoja Equatorial Guinea na Gabon, ambapo Stars inatakiwa kushinda mchezo huo ili kujihakikishia nafasi ya kucheza michuano hiyo.

Alisema kwa sasa Poulsen ambaye pia ni mkufunzi wa makocha wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) yuko Gambia ambapo anaendesha kozi ya wakufunzi na anatarajiwa kurejea nchini Septemba 24 kwa ajili ya maandalizi ya kikosi chake.

Wakati huohuo Wambura alisema Ligi Daraja la Kwanza inayoshirikisha timu 18 inatarajia kuanza mwezi ujao.

Alisema Kamati ya Mashindano inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, Ramadhan Nassib inatarajia kukutana Septemba 24 mwaka huu kuangalia mambo mbalimbali ya ligi hiyo.

Alisema moja ya mambo ambayo kamati hiyo itafanya ni kupitisha tarehe ya kuanza ligi hiyo pamoja na vituo.

No comments:

Post a Comment