TIMU ya Taifa ya Tanzania "Taifa Stars" imetolewa katika kinyang'anyiro cha kutafuta tiketi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Morocco mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Grand jijini Marrakech, Morocco. Jumapili jioni.
Morocco ndio waliokuwa wa kwanza kuona lango la Stars baada ya mshambuliaji wake machachari anayechezea klabu ya Arsenal ya Uingereza Maroune Chamakh kuipa timu yake bao la kuongoza dakika ya 20 kutoka mpira kuanza.
Bao hilo la Morocco liliongeza kasi kwa wachezaji wa Stars ambao mara kwa mara walikuwa langoni mwa wenyeji wao hao, juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 40 baada ya Abdi Kassim "Babi" kuisawazishia Stars bao hivyo kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimetoshana nguvu.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambualiana kwa zamu lakini ilikuwa ni Morocco ndio waliandika bao la pili kwa mpira wa adhabu dakika ya 68 kupitia kwa mchezaji wake Adel Taarabt kabla timu hiyo kuongeza bao la tatu dakika 89 hivyo kuzima ndoto za Stars kushiriki michuano hiyo itakayofanyika kwa ushirikiano baina ya Equatorial Guinea na Gabon 2012.
Kwa matokeo hayo Morocco inaungana na timu za Gabon, Equatorial Guinea ambao ndio waandaaji, Niger, Angola, Botswana, Ivory Coast, Ghana, Guinea, Mali, Senegal, Tunisia, Zambia, Burkina Faso, Sudan and Libya kuunda timu 16 zitakazoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) itakayofanyika 2012.
No comments:
Post a Comment