KLABU ya Chelsea inajiandaa kuwatema Salomon Kalou na Jose Bosingwa mwishoni mwa msimu mikataka yao itakapomalizika. Klabu hiyo itatangaza wachezaji inayowabakiza leo na majina yote ya wanaotemwa yatakuwa kwenye orodha moja na Didier Drogba. Nyota huyo Ivory Coast tayari amekwishasema ataondoka kwenye klabu hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka minane, ili akakabiliane na changamoto mpya. Bosingwa ana mkataba wa mwaka mmoja zaidi Stamford Bridge, lakini klabu imeamua kumtema. Kalou, ambaye pia anatokea Ivory Coast kama Drogba, alisajiliwa mwaka 2006 kutoka Feyenoord kwa dau la pauni Milioni 8. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, amecheza mechi zaidi ya 250, ikiwemo ile aliyoanza kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa kati ya Chelsea na Bayern Munich Jumamosi iliyopita, na amewafungia mabao 60 The Blues. Bosingwa, mwenye umri wa miaka 29, alisajiliwa na klabu hiyo baada ya kung'ara kwenye kikosi cha Ureno kwenye Euro 2008 baada ya Luiz Felipe Scolari, aliyekuwa kocha wa timu hiyo ya taifa kuchukuliwa kuikochi The Blues. Beki huyo alitua kutokea Porto kwa dau la pauni Milioni 16.2, na amecheza mechi 127 katika kipindi chake cha miaka minne ya kuwa na klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment