Thursday, May 3, 2012

KOCHA WA FIORENTINA ATIMULIWA BAADA YA KUMTWIKA NGUMI MCHEZAJI WAKE.

KOCHA wa Fiorentina ya Italia, Delio Rossi ametimuliwa baada ya kumpiga mchezaji wake katika mabishano ya kufanya mabadiliko. Mchezaji wa zamani wa majaribio Manchester United, Adem Ljajic alipingana na uamuzi wa kocha wake huyo kumtoa jana katika mechi ya Ligi Kuu ya nchini humo maarufu kama Serie A dhidi ya timu ya Novara. Rossi alikasirika na kuamua kumtoa nje na kumsukumia ngumi mshambuliaji huyo wa kimataifa kutoka Serbia. Rais wa Fiorentina, Andrea Della Valle alimfukuza kazi Rossi mara moja baada ya mechi hiyo, ingawa hadi sasa mrithi wake hajatangazwa. Tukio hilo lilitokea muda mfupi tu baada ya nusu saa ya mchezo, Fiorentina ikiwa imelala 2-0 dhidi ya wageni, ambao wanashika nafasi ya pili kutoka mkiani katika msimamo wa ligi hiyo. Rossi ambaye ameinoa klabu hiyo kwa muda wa miezi sita alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Sinisa Mihajlovic ambaye alitimuliwa Novemba mwaka jana kutokana na mwenendo mbaya wa klabu hiyo. Rossi anakuwa kocha wa 19 kufukuzwa timu za Ligi Kuu Italia msimu huu, na hivyo kuvunja rekodi ya kufukuzwa makocha 15 iliyowekwa msimu wa 1951-52.

No comments:

Post a Comment