LIPPI NYOTA YAWAKA CHINA.
|
Marcello Lippi. |
KOCHA wa klabu ya Guangzhou Evergrande ya nchini China, Marcello Lippi ameanza vyema kibarua chake hicho baada ya kufanikiwa kushinda mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu nchini maarufu kama Super League. Guangzhou ambao ni mabingwa watetezi wa taji la ligi hiyo waliifunga timu ya Qingdao Jonoon kwa bao 1-0 na kufanikiwa kukaa kileleni mwa ligi hiyo wakiwa alama nne zaidi ya timu inayofuatia. Lippi mwenye umri wa miaka 64 ambaye ni raia wa Italia alichukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo kutoka kwa Lee Jang-Soo raia wa Korea Kusini ambaye ameiongoza klabu hiyo kufikia hatua ya timu 16 bora katika michuano ya Kombe la Klabu Bingwa bara la Asia. Ushindi huo wa Lippi unakuja ikiwa ni siku tatu toka aanze kuifundisha timu hiyo ambapo amesema kuwa ni ushindi wa ajabu kwake kwani kipindi anafundisha klabu ya Juventus na baada timu ya taifa ya Italia mara zote amekuwa akipoteza mchezo wa kwanza. Lippi anaungana Nicolas Anelka ambaye alisajiliwa na klabu ya Shanghai Shenhua kuwa sehemu ya majina makubwa katika soka kujiunga na vilabu vya nchini humo baada ya mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa Jean Tigana kuondoka mwezi uliopita.
No comments:
Post a Comment