Friday, May 11, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF.

KIM KOCHA MPYA TAIFA STARS
Kim Poulsen ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania (Taifa Stars) kuanzia Mei 11 mwaka huu kuziba nafasi ya Jan Poulsen. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema Kim amepewa mkataba wa mwaka mmoja baada ya Shirikisho kuamua kutomuongezea mkataba Jan. Mkataba wa Jan uliokuwa wa miaka miwili unamalizika Julai 30 mwaka huu. Amesema kwa vile Taifa Stars inakabiliwa na mechi za mchujo za Kombe la Dunia raundi ya pili Kanda ya Afrika na mechi za mchujo za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN), TFF imeona ni lazima iwe na kocha mpya mapema kabla ya mkataba wa Jan kumalizika. Kim amekuwa nchini kwa mwaka mmoja sasa akifundisha timu za Taifa za vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) na miaka 20 (Ngorongoro Heroes), hivyo anawafahamu vizuri wa wachezaji wa Tanzania. Naye Kim ambaye Jumatatu (Mei 14 mwaka huu) atatangaza kikosi cha Taifa Stars ambacho Juni 2 mwaka huu kuivaa Ivory Coast katika mechi ya mashindano amesema yuko tayari kwa kazi hiyo na kusisitiza kuwepo ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali ili timu hiyo iweze kufanya vizuri.


RAMBIRAMBI MSIBA WA MWANDISHI RACHEL MWILIGWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mhariri wa Michezo wa gazeti la Mtanzania, Rachel Mwiligwa kilichotokea leo (Mei 11 mwaka huu) katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam. Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani Rachel kwa kipindi chote akiwa mwandishi na baadaye Mhariri alikuwa akifanya kazi nasi, hivyo mchango wake katika mpira wa miguu tutaukumbuka daima. TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Rachel, kampuni ya New Habari ambayo ndiyo inayomiliki gazeti za Mtanzania na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Rachel mahali pema peponi. Amina

TWIGA STARS, ZIMBABWE KUUMANA LEO
Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) na Zimbabwe zinapambana kesho (Mei 12 mwaka huu) katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Twiga Stars ambayo ilikuwa katika ziara ya mechi za kirafiki katika mikoa ya Dodoma na Mwanza imerejea leo (Mei 11 mwaka huu) jijini Dar es Salaam tayari kuikabili Zimbabwe. Ikiwa Mwanza jana ilicheza mechi ya kirafiki dhidi Rock City Queens, lakini mechi hiyo ilivunjika dakika ya 58 kutokana na mvua kubwa. Hadi mechi inavunjika, Twiga Stars ilikuwa ikiongoza kwa mabao 5-0. Kwa mujibu wa kocha wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa, mechi hiyo itakuwa kipimo kizuri kwao kabla ya kucheza mechi ya mashindano ya Afrika (AWC) dhidi ya Ethiopia. Mechi hiyo itachezwa Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa kabla ya kurudiana Dar es Salaam wiki mbili baadaye. Naye Kocha wa Zimbabwe, Rosemary Mugadza amesema amefurahi kupata mechi hiyo kwa vile anaamini Twiga Stars ni kipimo kizuri kwao kabla ya kucheza mechi yao ya AWC dhidi ya Nigeria. Twiga Stars na Zimbabwe zilishakutana mara mbili mwaka jana. Mara ya kwanza ilikuwa nusu fainali ya Kombe la COSAFA ambapo katika mechi hiyo iliyochezwa Julai 5 jijini Harare, Zimbabwe ilishinda kwa penalti 4-2. Mechi ya pili ilikuwa michezo ya All Africa Games (AAG) iliyofanyika Maputo, Msumbiji ambapo timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi wa kimataifa Judith Gamba kuanzia saa 10.30 jioni ni sh. 1,000 tu kwa sehemu zote isipokuwa VIP A ambayo ni sh. 10,000 na VIP B ambayo kiingilio chake ni sh. 5,000.

No comments:

Post a Comment