MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Lloyd Nchunga ameitisha Mkutano Mkuu wa wanachama utakaofanyika Julai 15, mwaka huu, Dar es Salaam. Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana huu, makao makuu ya klabu makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Nchunga alisema kwamba hayo yalifikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji, kilichofanyika jana, Dar es Salaam. Nchunga alisema kwamba kwa sasa Kamati ya Utendaji inakabidhi jukumu la kiufundi kwa Kamati ya Ufundi na benchi la Ufundi, ikiwemo usajili na uteuzi wa kocha mpya, atakayerithi mikoba ya Mserbia Kostadin Bozidar Papic aliyetimuliwa. Nchunga alisema amesikitishwa na timu kushindwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na sasa maandalizi yanaanza mara moja, kuhakikisha msimu ujao Yanga inarejesha heshima. Alisema maandalizi hayo yatahusu timu ya wakubwa na timu za vijana pia. Aidha, Mwenyekiti huyo alisema katika kurejesha umoja na amani ndani ya klabu hiyo, iliyopotea baada ya klabu kufungwa 5-0 na wapinzani wao wa jadi, Simba, Mei 6, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu, Kamati ya Utendaji imepanga kukutana na wadau mbalimbali wa klabu. Alisema lengo la kukutana na wadau hao ni kubadilishana mawazo na uzoefu katika kuendesha klabu, ili msimu ujao mambo yawe safi tena. Alisema kwa kuanzia, Kamati ya Utendaji itakutana na Wazee wa klabu wa nchi nzima na ametoa wito kwa wazee walio nje ya Dar es Salaam kujitahidi kufika klabu Jumapili asubuhi kwa ajili ya Mkutano huo. Kuelekea Mkutano Mkuu, Nchunga alisema wanachama wote wanatakiwa kulipia ada za uanachama wao, ili waweze kushiriki. Mapema mkutano huo ulichelewa kuanza kama ilivyopangwa kuanza saa 5:00 asubuhi, kutokana na kuibuka kundi la wanachama wasiopungua 100 ambao wanadaiwa kutumiwa na wapinzani wa uongozi kuvamia makao makuu ya klabu na kufanya vurugu. Hata hivyo, jeshi la polisi lilishusha vikosi vyake hapo na kutuliza vurugu hizo, hatimaye Nchunga akafanikiwa kuzungumza na waandishi. Hamkani si shwari Yanga- yapata mwezi mmoja sasa na mambo yaliharibika mara tu baada ya waliokuwa Wajumbe wa Kamati ya Mashindano na Usajili, Seif Ahmad ‘Seif Magari’ na Abdallah Bin Kleb kujiuzulu siku chache kabla ya mechi na Simba SC. Kufuatia hali hiyo, viongozi wa Baraza la Wazee la klabu wakiongozwa na Katibu wao Mkuu, Mzee Ibrahim Ally Akilimali waliibuka kuomba wakabidhiwe timu, kwa kuwa Nchunga amechemsha na hali ni mbaya. Nchunga aliwataka Wazee hao, kumueleza vyanzo vyao vya mapato, vitakavyowawezesha kuendesha timu ndipo awakabidhi, lakini wakashindwa kufanya hivyo. Nchunga aliipeleka timu kambini Bagamoyo na Jumapili ya Mei 6, akaishusha Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikapigwa 5-0 na tangu wakati huo imekuwa ‘Mtafutano Jangwani’. Mara tu baada ya mechi, Nchunga alidai kuna wachezaji walitumiwa na wapinzani wake kuihujumu timu hadi ikala kipigo hicho na akasema wanafanya uchunguzi wa kina ili kuwajua wahusika kabla ya kuchukua hatua kali, ikiwemo kuwafukuza waliohusika.
No comments:
Post a Comment