Thursday, August 2, 2012
MISRI, SENEGAL ZATINGA ROBO FAINALI OLIMPIKI.
WAWAKILISHI wa Afrika katika soka kwenye michuano ya Olimpiki inayoendelea jijini London timu za Misri na Senegal zimefanikiwa kusonga mbele katika michuano hiyo baada ya kutinga hatua ya robo fainali. Misri waliingia katika hatua baada ya kuichapa bila ya huruma timu ya Belarus kwa mabao 3-1 na kutinga hatua hiyo ambapo sasa watakutana na timu ya Japan katika mchezo utakaochezwa Juamosi katika Uwanja wa Old Traford jijini Manchester. Senegal nao walitinga hatua hiyo baada ya kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE bao ambalo lilisawazishwa na mshambuliaji nyota wa timu hiyo Moussa Konate ambapo mpaka sasa amefunga mabao manne katika michuano hiyo. Nchi hiyo sasa itapambana na Mexico ambao wanaongoza kundi B baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Switzerland huku wenyeji wa michuano hiyo Uingereza wenyewe watacheza na Korea Kusini. Timu inayopewa nafasi kubwa ya kunyakuwa medali ya dhahabu kwa mara kwanza katika michuano hiyo Brazil wenyewe watamenyana na Honduras katika robo fainali ya michuano hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment