Tuesday, February 5, 2013

GAZZA APELEKWA NCHINI MAREKANI KWA MATIBABU YA ULEVI.

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Uingereza, Paul Gascoigne maarufu kama Gazza amepelekwa nchini Marekani kwa matibabu ikiwa ni masaa 24 baada ya wakala wake kubainisha kuwa nyota huyo afya yake iko hatarini kutokana na ulevi uliopindukia. Gazza ambaye amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya ulevi kwa miaka mingi alionekana akiongea kwa kutetemeka mwili mzima wakati alipoalikwa katika shughuli ya kijamii jijini Northampton Alhamisi iliyopita. Picha za video za nyota huyo zilichapishwa katika mtandao wa gazeti la The Sun nchini humo wakimkariri wakala wake Terry Baker akidai kuwa mteja wake huyo alikuwa akihitaji msaada wa haraka kutokana na maisha yake kuwa hatarini. Katika taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari imedai kuwa nyota huyo wa zamani wa klabu za Tottenham Hotspurs, Lazio, Rangers na Newcastle alikubali mwenyewe kwa hiari yake kulazwa katika kliniki inayoshughulika na watu wenye matatizo hayo huko Marekani. Gazza ambaye anahesabika kama mmoja wa wachezaji wenye vipaji zaidi kuwahi kutokea nchini Uingereza aliichezea nchi hiyo mechi 57 za kimataifa.

No comments:

Post a Comment