Wednesday, February 6, 2013
LANGALANGA 2013: HAMILTON APATA AJALI AKIWA KATIKA MAJARIBIO.
DEREVA nyota wa mashindano ya magari ya langalanga, Lewis Hamilton ameanza vibaya siku yake ya kwanza ya majaribio akiwa na timu yake mpya ya Mercedes baada ya kupata ajali kwa kugonga ukuta baada ya mzunguko wa 15 kwasababu ya matatizo ya breki. Hamilton ambaye ni bingwa wa dunia wa mashindano wa 2008 alipoteza mwelekeo na gari lake akiwa katika mzunguko wa mwisho katika barabara za Jerez zilizoko kusini mwa Hispania. Dereva alitoka salama katika ajali hiyo baada ya kugonga ukuta wa matairi uliokuwepo pembeni ya barabara hizo, huku timu yake ya Mercedes ikidai kuwa gari hilo lilikata breki zake za nyuma. Hamilton alijaribu kulisimamisha kwa kutumia breki za mbele lakini ilishindikana kuukwepa ukingo wa barabara hiyo, timu yake inajaribu kuanza kufanya uchunguzi kugundua chanzo kilichosababisha breki za nyuma kushindwa kufanya kazi. Hili ni tatizo la pili kutokea kwa Mercedes katika siku mbili za majaribio baada ya dereva mwenzake Hamilton, Nico Rosberg kushindwa kuendelea na majaribio katika mzunguko wa 11 kutokana matatizo ya umeme yaliyotokea katika lake. Hamilton mwenye umri wa miaka 28 alisaini mkataba wa miaka mitatu na kampuni ya Mercedes Septemba mwaka jana baada ya kuondoka McLaren ambako ndiko alipoanza kushiriki mashindano hayo mwaka 2007.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment