
Tuesday, March 19, 2013
JORGINHO KUINOA FLAMENGO.
KLABU ya Flamengo ya Brazil imemtaja beki wa zamani wa kimataifa wa nchi hiyo na klabu ya Bayern Munich Jorginho kuchukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo maarufu. Jorginho ambaye alinyakuwa Kombe la Dunia mwaka 1994 akiwa katika kikosi cha Brazil amewahi kufanya kazi kama msaidizi wa kocha wa nchi hiyo Dunga kuanzia mwaka 2006 mpaka 2010. Kocha huyo amechukua mikoba ya Dorival Junior ambaye alitimuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kukataa kupunguziwa mshahara wake na klabu hiyo. Katika taarifa ya klabu hiyo iliyotumwa katika mtandao wake imesema wana imani na Jorginho kuipa mafanikio klabu hiyo pamoja na matatizo ya kifedha yaliyopo ambayo ndio yamepelekea baadhi ya wafanyakazi kupunguziwa mishahara. Akiwa mchezaji Jorginho alijiunga na Flamengo akiwa na umri wa miaka 20 na kuitumikia klabu hiyo kwa miaka miatano kabla ya kwenda Bayer Leverkusen na baadae Bayern. Jorginho pia alikuwepo katika kikosi cha Brazil kilichoshiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1990 na alikuwa sehemu sehemu ya kikosi cha nchi hiyo kilichonyakuwa michuano ya Kombe la Amerika mwaka 1989.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment