Friday, March 15, 2013

VITUKO VYA MASTAA: LEONARDO PROPOSES LIVE ON AIR.

Mkurugenzi wa michezo wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG ya Ufaransa Leonardo amemuomba mchumba wake ambaye ni mtangazaji wa luninga ya Sky nchini Italia Anna Billo kumuoa moja kwa moja hewani baada ya upangaji wa ratiba ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Billo ambaye alikuwa akitangaza matangazo ya moja kwa moja ya Sky kwa kiitaliano katika shughulia hiyo ya upangaji ratiba nchini Switzerland alikuwa akiongea na Leonardo kuhusu PSG kupangiwa mchezo wao robo fainali na Barcelona wakati akimuuliza kama ana swali lolote alitaka kuuliza. Kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Brazil na pia aliyewahi kuzinoa timu za AC Milan na Inter alitumia mwanya huo kwa kumuuliza Anna kama anataka kuolewa naye swali ambalo lilikuwa la ghafla lilimfanya mtangazaji huyo kuona haya kidogo. Billo ambaye amezaa mototo mmoja wa kiume na Leonardo aliendelea na kujifanya kuipotezea huku watu waliokuwepo studio wakicheka lakini nyota huyo alirudia tena swali lake kwa msisitizo na kudai kuwa alikuwa akisubiria jibu hapohapo. Akiwa katika mshangao huku akitabasamu Billo alimjibu Leonardo sawa tutaona huku akiendelea kutabasamu kabla ya kukatishwa kwa kipindi kwa ajili ya matangazo ya biashara. Miaka mitano iliyopita aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Raymond Domenech alifanya tukio kama hilo kwa kuomba kumuoa mtangazaji wa luninga ya Ufaransa Estelle Denis katika mahojiano ya moja kwa moja dakika chache baada ya nchi hiyo kutolewa katika mzunguko wa kwanza wa michuano ya Ulaya 2008 kwa kuchapwa mabao 2-0 na Italia.

No comments:

Post a Comment