Tuesday, April 23, 2013

KANSELA MERKEL ASONONESHWA NA KASHFA YA UKWEPAJI KODI YA HOENESS.

KANSELA wa Ujerumani Angela Merkel amefadhaishwa na kashfa ya kukwepa kodi inayomkabili rais wa klabu ya Bayern Munich, Uli Hoeness, huku Hoennes mwenyewe akisema hatajiuzulu wadhifa wake kupisha uchunguzi unaoendelea dhidi yake. Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert, amesema kwamba watu wengi nchini Ujerumani wamefadhaishwa na Hoennes, na hivyo ndivyo alivyo pia Kansela Merkel. Kwa mujibu wa Seibert, Kansela Merkel amefadhaishwa zaidi kutokana na ukweli kwamba Hoeness amekuwa kielelezo chema kwa Ujerumani, kwani sio tu kwamba anaongoza klabu bora kabisa ya mpira, bali pia amekuwa akiunga mkono jithada kadhaa za maendeleo, ukiwemo mradi wa kuwajumuisha wageni kwenye jamii ya Ujerumani. Mwishoni mwa wiki, Hoeness alinukuliwa na gazeti la kila wiki la Focus akisema kwamba aliripoti mwenyewe kwa mamlaka juu ya akaunti yake ya fedha kwenye benki moja nchini Switzerland hapo mwezi Januari. Waendesha mashitaka wamekiri kwamba wameanzisha uchunguzi huo kufuatia ripoti iliyopelekwa kwao na Hoeness mwenyewe kupitia mshauri wake wa masuala ya fedha. Hata hivyo, Hoeness, mwenye umri wa miaka 61, amesema hana mpango wowote wa kujiuzulu kutokana na tuhuma hizo za kukwepa kodi. 

No comments:

Post a Comment