KOCHA wa timu ya taifa ya Nigeria, Stephen Keshi amewataka wachezaji wake kuwa makini zaidi bindi wafikapo langoni mwa wapinzani wao baada ya kukosa nafasi kadhaa katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Tahiti ambao walishinda kwa mabao 6-1. Pamoja na ushindi huo mnono waliopata jana usiku, Nigeria maarufu kama Super Eagles walipoteza nafasi nyingi za wazi na kushindwa kumtungua mabao mengi zaidi kipa wa Tahiti Xavier Simin. Mabingwa hao wa Afrika kwasasa wanaongoza kundi B kwa wastani mzuri wa mabao hata hivyo Keshi amesisitiza kuwa pamoja na makosa hayo lakini amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake na anategemea kuendelea hivyo katika mchezo dhidi ya Uruguay.
Katika mchezo huo uliopigwa huko Belo Horizonte mashabiki waliohudhuria mchezo huo walionyesha kuwa upande wa Tahiti na mabao ya Nigeria hayakuonyesha kuwakuna mashabiki hao lakini Keshi hajali suala hilo. Keshi amesema unapokuwa mchezaji wa kulipwa mambo kama hayo ni ya kawaida kukutana nayo kitu cha msingi ni kuhakikisha unapata matokeo muhimu ili uweze kusonga mbele. Michuano hiyo inaendelea tena kesho ambapo wenyeji Brazil watakwaana na Waamerika Kusini wenzao Mexico katika Uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro.
No comments:
Post a Comment