Thursday, July 4, 2013

KIPIGO CHA IVORY COAST CHAIPOROMOSHA TANZANIA VIWANGO FIFA.

KIPIGO cha mabao 4-2 ilichopata timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kutoka kwa Ivory Coast katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 uliochezwa mwezi uliopita kimechangia kuiporomosha katika viwango vya ubora duniani. Tanzania ambayo mwezi uliopita ilikwea kwa nafasi tisa kutoka nafasi ya 116 waliyokuwepo mpaka nafasi ya 109, katika orodha zilizotolewa mwezi huu na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA imeonyesha kuporomoka kwa nafasi 12 mpaka nafasi ya 121. Kwa upande wa Afrika Ivory Voast bado wameendelea kuongoza kwa kushika nafasi ya13 wakifuatiwa na Ghana waliopo katika nafasi ya 24 baada ya kuporomoka kwa nafasi tatu huku Mali wakifuatia katika nafasi ya 28 baada ya kuporomoka kwa nafasi tano. Wengine kwa upande wa Afrika ni Algeria waliopo katika nafasi ya 34 baada ya kupanda kwa nafasi moja na tano bora inafungwa na mabingwa Afrika Nigeria waliopo katika nafasi ya 35 baada ya kuporomoka kwa nafasi nne. Kwa upande wa orodha hizo duniani, Hispania bado wameendelea kuwa vinara wakifuatiwa na Ujerumani huku katika nafasi ya tatu kukiwa na ingizo jipya Colombia waliopanda kwa nafasi tatu na kuiondoka Argentina ambao wako katika nafasi ya nne. Nafasi ya tano katika orodha hizo inashikiliwa na Uholanzi huku mabingwa wapya wa Kombe la Shirikisho Brazil wakirejea tena katika 10 bora baada ya kukwea kwa nafasi 13 mpaka nafasi ya tisa.


No comments:

Post a Comment