MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Liverpool, Luis Suarez ameamriwa kufanya mazoezi peke yake na meneja wa klabu hiyo Brendan Rodgers ambaye amedai kuwa mchezaji huyo ameshindwa kuonyesha heshima kwao. Rodgers pia alikana madai kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay aliahidiwa uhamisho katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi kama Liverpool ingeshindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Suarez mwenye umri wa miaka 26 amepanga kuwasilisha barua ya kuomba kuondoka wiki hii kama akizuiwa. Rodgers amesisitiza kuwa hakuna ahadi yoyote iliyowekwa au iliyovunjwa hivyo madai hayo ni kuivunjia heshima klabu hiyo ambayo imekuwa ikijitahidi kumpa kila kitu. Suarez ambaye anataka kwenda klabu inayoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa alitoa kauli hiyo baada ya kuona Liverpool wamekataa ofa mbili zilizotolewa na Arsenal kwa ajili ya kumsajili ikiwemo ile ya paundi milioni 40 ambayo inamruhusu kuanza mazungumzo baada ya kufikia vigezo vya mkataba wake.

No comments:
Post a Comment