Monday, January 13, 2014

FIKRA HURU: NIGERIA WALITAWALA TUZO ZA CAF...

PAMOJA na Nigeria kuikosa zawadi muhimu ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika katika sherehe za utoaji tuzo zilizoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF kwa kuchukuliwa na Yaya Toure wa Ivory Coast hakuna shaka kwamba Nigeria walitawala tuzo hizo. Nigeria walitawala tuzo hizo kwa kunyakuwa sita katika vipengele 11 huku mtu wa kwanza katika orodha hizo akiwa kocha wa timu ya taifa ya Nigeria alipewa tuzo ya kocha bora wa mwaka kutokana na mafanikio aliyopata. Tuzo nyingine kwa nchi hiyo ilikwenda kwa mchezaji chipukizi wa nchi hiyo Kelechi Iheanacho ambaye alichukua tuzo hiyo mbele chipukizi wenzake wengine wawili kutoka Ghana na Misri. Mashabiki wa Nigeria nao hawakutoka kapa kwani walipewa tuzo ya CAF Fair Play kwa utulivu wao wakati wakiishangilia nchi yao wakati timu ya taifa Super Eagles ilipewa tuzo ya timu ya taifa ya mwaka na kuzipita Ethiopia na Burkina Faso waliokuwa katika kinyang’anyiro hicho. Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 nao walipewa tuzo yao kwa kuwa timu bora ya mwaka kwa vijana wa umri huo baada ya kufanikiwa kunyakuwa taji la michuano ya Kombe la Dunia mwaka jana. Kwa mlolongo huo ambao umepelekea CAF kuteua wachezaji wanne wa nchi hiyo pamoja na kocha kuongoza kikosi cha wachezaji nyota wa bara la Afrika hakuna shaka kwamba Nigeria walitawala tuzo hizo zilizofanyika Alhamisi iliyopita.

No comments:

Post a Comment