KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi Clarence Seedorf anatarajiwa kuwa kocha mpya wa klabu ya AC Milan baada ya kuamua kutundika daruga jana. Seerdorf mwenye umri wa miaka 37 ambaye hana uzoefu wa muda mrefu katika kufundisha aliwaambia waandishi wa habari adhma yake ya kustaafu kucheza katika klabu ya Botafogo ya Brazil ambayo alijiunga nayo mwaka 2012 akitokea Milan. Akihojiwa wakati akiaga, Seerdorf amesema uzoefu wake wote alioupata wakati akiwa kocha mchezaji wa Botafogo utamsaidia katika safari yake mpya ya ukocha katika timu ya Milan. Wakala wa Seedorf, Deborah Martin amesema mteja wake huyo amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu kuchukua nafasi ya Massimiliano Allegri aliyetimuliwa mapema Jumatatu kufuatia matokeo mabaya yaliyoiandama timu hiyo. Enzi zake nyota huyo aliweka historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kushinda taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya akiwa na vilabu vitatu tofauti ambavyo ni Ajax Amsterdam mwaka 1995, Real Madrid mwaka 1998 na AC Milan mwaka 2003 na 2007.

No comments:
Post a Comment