BINGWA mtetezi wa michuano ya wazi ya Australia, Victoria Azarenka amesisitiza hajali Serena Williams kupewa nafasi ya kunyakuwa taji la michuano hiyo na kudai kuwa ana hamasa ya hali ya juu ya kumfunga nyota huyo anayeongoza katika orodha za ubora wa mchezo huo duniani kwa upande wa wanawake. Williams amekuwa katika kiwango cha juu ambapo amepoteza michezo mitano pekee mwaka jana huku akimfunga Azarenka katika mechi ya mwisho ya kujipima nguvu katika michuano ya ya kimataifa ya Brisbane mwezi huu. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo Azarenka amesema yeye hajali kwani suala la hilo huwa linakuzwa na vyombo vya habari na wao kazi yao kucheza tenisi kwa kiwango chako chote uwanjani. Azarenka amesema Williams sio mchezaji pekee katika hayo kwani kila mpinzani atakayekutana amejiandaa kwa ajili ya michuano hiyo hivyo inabidi kujiandaa kiakili katika kila mchezo unaocheza ili kuhakikisha unafikia lengo lako. Azarenka anatarajiwa kucheza mechi yake ya ufunguzi na Johanna Larsson wa Sweden jijini Melbourne kesho.

No comments:
Post a Comment