Thursday, June 12, 2014

KIBABU BLATTER AKOMAA, ADAI ATAGOMBEA KWA KIPINDI KINGINE CHA TANO.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter anatarajiwa kugombea nafasi hiyo kwa kipindi kingine baada ya mkutano mkuu wa shirikisho hilo kutounga mkono kikomo cha muda na umri kwa viongozi. Blatter mwenye umri wa miaka 78 katika kipindi cha karibuni amekuwa akidokeza suala la kuongeza kipindi kingine kuliongoza shirikisho hilo kwa madai kwamba hajamaliza yale aliyotaka kuyafanya. Rais huyo pia alilishambulia gazeti la Sunday Times la Uingereza kwa kuwaita wabaguzi wa rangi baada ya kuibua tuhuma za rushwa zilizopelekea Qatar kupewa nafasi ya kuandaa michuano ya Kombe la Dunia 2022 hivyo kuibua hisia tofauti miongoni mwa viongozi wa juu wa Shirikisho la Soka Ulaya. Pamoja na hayo kura zilizopigwa katika mkutano huo kupinga suala la kikomo cha muda na umri wa kuongoza shirikisho hilo, kinaonyesha ni jinsi gani Blatter alivyokuwa na nguvu na kuungwa mkono na wanachama wake duniani kote. Mara baada ya mkutano huo Blatter amesema anajua muda wake unamalizika Mei 29 mwakani katika uchaguzi utakaofanyika jijini Zurich lakini mipango yake bado haijamalizika huku akiwaambia wajumbe kuwa kwa pamoja wataweza kuitengenza FIFA mpya.

No comments:

Post a Comment