MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi alipigwa na butwaa wakati wa mazoezi ya timu hiyo jana wakati shabiki mmoja alipovamia uwanjani na kudhani alikuwa mchezaji mwenzake wa zamani wa Barcelona na rafiki yake Ronaldinho. Kikosi cha Argentina kilikuwa kinafanya mazoezi mbele ya maelfu ya mashabiki sambamba na vyombo vya habari katika Uwanja wa Independent uliopo huko Belo Horizonte, ambapo mara nyingi Ronaldinho amekuwepo akiwa na timu ya Atletico Mineiro. Baada ya kufanya mazoezi mepesi ya kukimbia, kikosi cha timu hiyo kilijigawanya kwa makundi madogo kwa ajili ya kuendelea na mazoezi mengine ambapo mwishoni mamia ya mashabiki hao waliruka uzio na kuingia uwanjani kwa ajili ya kuwapa mikono mashujaa wao hao. Wengine wa mashabiki hao walikuwa wakikimbia eneo alilokuwepo Messi lakini nyota huyo alistaajabishwa na shabiki mmoja aliyefanana kila kitu na Ronaldinho. Akihojiwa shabiki huyo Robinson Oliveira aliuambia mtandao wa Goal kuwa wakati Messi alipomuona alishtuka kwasababu alidhani ni Ronaldinho wa kweli na alimwambia kuwa hahitaji kukimbia katika eneo la uwanja ili aweze kumuona. Olivier aliendelea kudai kuwa baada ya kugundua hakuwa Ronaldinho aliyemdhania alibaki ameshangaa huku akicheka na baadae kushikana mikono na kukumbatiana kabla walinzi hawajamtoa katika eneo hilo. Argentina inatarajiwa kuanza kutupa karata yake ya kwanza kwa mchezo dhidi ya Bosnia katika Uwanja wa Maracana, Jumapili.

No comments:
Post a Comment