Wednesday, June 4, 2014

SCOLARI BADO HAJARIDHIKA NA KIWANGO CHA BRAZIL.

KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luiz Felipe Scolari amedai kuwa bado iko nafasi kwa timu yake kufanya vizuri zaidi kuelekea katika mchezo wao wa ufunguzi wa Kombe la Dunia dhidi ya Croatia utakaochezwa Juni 12 mwaka huu. Jana timu hiyo ilifanikiwa kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 katika chezo wa kirafiki dhidi ya Panama mabao ambayo yalifungwa na nyota wake Neymar, Dani Alves, Hulk na Willian. Lakini pamoja na ushindi huo na mchezo murua walioonyesha, Scolari bado anadhani kuna sehemu za kufanyia marekebisho ili kuziboresha zaidi kabla ya kuanza kwa michuano hiyo. Scolari amesema amefurahishwa na kikosi chake kutowaachia wapinzani wao kuwafanyia mashambulizi ya ghafla lakini bado anaona wana safari ndefu na kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha wanafanya katika michuano iliyopo mbele yao. Mechi zingine za kirafiki za kimataifa zilizochezwa jana ni pamoja na wawakilishi kutoka Afrika katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu Nigeria ambao walitoshana nguvu ya bila kufungana na Ugiriki, Bosnia wao wakaitandika Mexico bao 1-0 huku Switzerland wakiitambia Peru kwa kuifunga mabao 2-0.

No comments:

Post a Comment