KLABU ya Bayern Munich imefanikiwa kumsajili mchezaji chipukizi Felix Gotze ambaye ni ndugu yake na shujaa wa Ujerumani Mario Gotze, kutoka klabu ya Borussia Dortmund. Felix aliyekuwa akichezea timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Dortmund msimu uliopita ameamua kuhamia kwa mabingwa hao wa Bundesliga ili kufuata mfano wa kaka yake. Mkurugenzi wa timu ya vijana ya Bayern Michael Tarnat alithibitisha taarifa za kinda huyo kuhamia katika timu hiyo. Felix mwenye umri wa miaka 16 anakuwa ndugu wa tatu katika familia ya Gotze kuondoka Borussia Dortmund baada ya Fabian kuhamia Mainz Januari mwaka 2010 na Mario kwenda Bayern katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka jana. Mario Gotze amekuwa akipambana kucheza kwa kiwango cha juu akiwa Bayern kulingana na thamani yake aliyonunuliwa ya euro milioni 37 mwaka jana lakini amefanikiwa kung’ara katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu kwa kufunga bao lililoipa ubingwa Ujerumani.

No comments:
Post a Comment