SHIRIKISHO la Soka wa nchini-TFF limedai kutotambua mabadiliko ya uongozi ndani ya Coastal Union yanayodaiwa kufanywa na mkutano wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika hivi karibuni. Katika taarifa ya shirikisho hilo iliyotumwa na Ofisa Habari wake Boniface Wambura, TFF imesema wao wanatambua uongozi wa Coastal Union uliochaguliwa na mkutano wa uchaguzi wa klabu na ndio wataendelea kufanya nao kazi, na sio uongozi mwingine wowote ule. Shirikisho hilo limewakumbusha wanachama wakewakiwemo Coastal Union kuheshimu katiba ya TFF pamoja na katiba zao, kwani hazitambui mapinduzi ya uongozi wala kamati za muda za utendaji. TFF inafanya kazi za kamati za utendaji zilizopatikana kwa njia ya uchaguzi tu. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa tayari TFF imepokea barua kutoka kwa Kaimu Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mnguto ikilalamikia kusimamishwa kwake na wanalifuatilia suala hilo kwa kina, na ikibainika kuwa kuna viongozi wamehusika katika mapinduzi hayo watafikishwa katika vyombo husika kwa hatua zaidi.
No comments:
Post a Comment