Sunday, December 14, 2014

RIBERY AFIKIRIA KUMALIZIA SOKA LAKE ASIA AU MAREKANI.

WINGA mahiri wa klabu ya Bayern Munich, Franck Ribery amebainisha kuwa anaweza kwenda kucheza Marekani, Qatar au Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE kabla ya kustaafu rasmi soka. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 kwasasa ni mchezaji muhimu katika kikosi cha kwanza cha Bayern iliyo chini ya Pep Guardiola huku mkataba wake ukitarajiwa kumalizika Juni mwaka 2017. Hata hivyo wakati Robery akisisitiza kuwa hana mpango wa kuhamia katika klabu yeyote ya barani Ulaya sasa ameweka wazo la kutafuta changamoto katika timu za bara la Asia au Marekani. Akihojiwa Ribery amesema amekuwa hapo kwa miaka nane hivyo anaweza kusema Bayern na yeye ni kama watu waliofunga ndoa. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa amenunua nyumba hapo na mtoto wake wa kiume amezaliwa hapo huku mwingine wa kike akikulia hapo na wanazungumza Kijerumani kuliko yeye. Kutokana na hilo Ribery amesema itakuwa vigumu kwake kucheza katika klabu nyingine barani Ulaya kwani ametokea kuipenda sana Bayern, ingawa hata akaongeza kuwa anaweza kutafuta changamoto nyingine barani Asia na Marekani kabla ya kustaafu.

No comments:

Post a Comment