KIUNGO wa kimataifa wa Cameroon na klabu ya West Ham United Alex Song ametangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya kuenguliwa katika kikois cha timu ya taifa ya nchi hiyo kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon. Song mwenye umri wa miaka 27 ambaye yuko kwa mkopo West Ham akitokea Barcelona, sasa atakuwepo katika kikosi cha timu yake mwezi huu baada ya mazungumzo ya kurejea kwenye kikosi cha Cameroon kushindikana. Nyota huyo alithibitisha taarifa hizo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram akidai kuwa pamoja na uamuzi aliochukua lakini mapenzi na nchi yake hayataweza kubadilika kamwe. Song aliendelea kudai kuwa sasa anataka kuhamishia nguvu zake katika klabu yake na kuisadia kuipa mafanikio waliyojiwekea. Song hajaitumikia Cameroon toka alipotolewa nje katika mchezo dhidi ya Croatia katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka jana.

No comments:
Post a Comment