Tuesday, February 17, 2015

TETESI ZA USAJILI ULAYA: UNITED YAMUWINDA NEYMAR MPYA KUTOKA FLUMINESE, ARSENAL YAMCHACHAMALIA DYBALA, CHELSEA NA UNITED KUTOANA MACHO KWA VERANE.

KATIKA habari za tetesi za usajili klabu ya Manchester United iko tayari kutoa kitita cha euro milioni 6.5 kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa klabu ya Fluminese Kenedy ambaye anatabiriwa kuwa Neymar mpya. Nyota huyo wa Brazil amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na United ingawa wanakabiliwa na upinzani kutoka kwa klabu ya Inter Milan. Katika taarifa nyingine inayoihusu United ni kuwa rais wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez amedai yuko tayari kupokea fedha kwa ajili ya timu itakayotaka kumsajili Cristiano Ronaldo. Kumekuwa na tetesi mbalimbali kuhusu kurejea kwa nyota huyo Old Trafford hivyo taarifa hizo zinaweza kuwa muhimu kwa United kufikia lengo lao. Klabu ya Arsenal inaongoza mbio za kutaka kumsajili mshambuliaji wa klabu ya Palermo Paulo Dybala ambapo viongozi wake wanajipanga kukutana na rais wa timu hiyo Maurizio Zamparini. Arsenal wanataka kutenga kitita cha euro milioni 40 kwa ajili ya nyota huyo wa kimataifa wa Argentina kabla ya majira ya kiangazi. Klabu ya West Ham United nayo imeingia katika kinyang’anyiro cha kuwania kumsajili mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Paris Saint-Germain Nene. Nene mwenye umri wa miaka 33 kwasasa ni mchezaji huru baada ya kusitisha mkataba wake na klabu ya Al Gharafa na pia anawindwa na klabu ya West Bromwich Albion. Klabu ya Paris Saint-Germain bado ina matumaini ya kumsajili Eden Hazard pamoja na nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji kusaini mkataba mpya wa muda mrefu na Chelsea. Klabu za Chelsea na Manchester United ziko katika mapambano ya kumuwania Rafael Verane. Beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa anaonekana hana furaha katika klabu ya Real Madrid kutokana na kupata muda mchache wa kucheza na yuko tayari kuondoka, ingawa klabu hizo za Ligi Kuu zitalazimika kutoa paundi milioni 25 kama watamuhitaji.

No comments:

Post a Comment