MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Ivory Coast, Didier Drogba amebainisha mtoto wake mkubwa wa kiume aitwaye Isaac mwenye umri wa miaka 16 hana mpango wa kulitumikia taifa hilo lililopo Afrika ya Magharibi kama atakuja kuwa mchezaji wa kulipwa. Mshambuliaji huyo wa Chelsea mwenye umri wa miaka 36, mara nyingi amekuwa akieleza kutamani kumuona mwanae akicheza soka na pia timu ya taifa ya Ivory Coast. Akihojiwa jana, Drogba amesema wakati alipomuuliza mwanae ni nchi gani anayopenda kuichezea alimjibu kuwa napenda kuitumikia Uingereza. Isaac amezaliwa jijini Paris mwaka 1999 na ana uraia wa Ufaransa kwa mujibu wa baba yake lakini familia yao inaishi Uingereza toka Drogba alipojiunga na Chelsea akitokea Marseille mwaka 2004. Drogba amesema hajui kwanini Isaac hataki kuichezea Ivory Coast na kama itafika siku ya yeye kuchagua taifa la kuchezea atamuachia liwe chaguo lake.

No comments:
Post a Comment