MENEJA wa Inter Milan, Roberto Mancini amesema klabu hiyo inahitaji muda kujijenga kama wanataka kurudi tena katika ushindani kwenye Ligi Kuu ya Italia maarufu kama Serie A. Inter wameshindwa kunyakuwa taji la Serie A toka mwaka 2010, huku wakiwa na msimu mbaya toka Mancini alipochukua mikoba Novemba mwaka jana baada ya Walter Mazzari kutimuliwa. Pamoja na kutarajiwa kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara nyingine, Mancini amesema ana uhakika rais Erick Thohir atakiweka pamoja kikosi ambacho kinaweza kumaliza utawala wa Juventus ambao wanatarajiwa kunyakuwa taji la nne mfululizo la Serie A. Mancini amesema wanatakiwa kuimarika na ili waweze kufikia malengo hayo itahitaji muda kwa kutengeneza wachezaji ambao watakaa pamoja kwa kipindi kirefu. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa rais analifahamu hilo na anaunga mkono kuwa ili kuunda kikosi imara inahitaji muda. Inter kwasasa wako nafasi ya tisa katika msimamo wa Serie A wakiwa alama tatu nyuma ya Sampdoria wanaoshika nafasi ya tano ambayo inaweza kuwawezesha kushiriki mashindano ya Europa League.
No comments:
Post a Comment