Monday, December 7, 2015

LIGI YA MABINGWA ULAYA KUENDELEA KESHO.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa mechi za makundi kuelekea hatua ya timu 16 bora. Katika mechi za kesho vinara wa kundi A Real Madrid watakuwa wenyeji wa Malmo ya Sweden huku Paris Saint-Germain-PSG ya Ufaransa wao wakiwakaribisha Shakhtar Donetsk ya Ukraine ambapo timu zote hizo Madrid na PSG tayari zimeshafuzu hatua inayofuata. Manchester United ambao Jumamosi iliyopita walilazimishwa sare ya bila kufungana na West Ham United katika mchezo wa Ligi Kuu watakuwa na kibarua kizito katika kundi B pale watakaposafiri kuelekea Ujerumani kuchuana na Wolfsburg huku PSV Eindhoven ya Uholanzi wao wakiwa wenyeji wa CSKA Moscow ya Urusi. Timu tatu za United, Wolfsburg na PSV zote zina nafasi sawa katika kundi hilo kama wakifanikiwa kushinda mechi zao hizo za mwisho kesho. Kwa upande wa kundi C timu za Atletico Madrid na Benfica tayari zimeshajikatia tiketi ya kusonga mbele lakini wao kila mmoja atakuwa akitafuta ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kumaliza katika nafasi ya kwanza wakati watakapokutana kesho huku Galatasaray ya Uturuki wakichuana na FC Astana wakigombea nafasi ya tatu kwenda kushiriki michuano ya Europa League. Matajiri wa Uingereza Manchester City wao watajitupa uwanjani wakimalizia mchezo wao mwisho wa kundi D dhidi ya Borussia Monchengladbach wakiwa tayari na uhakika wa kusonga hatua inayofuata huku vinara wa kundi hilo Juventus nao wakipepetana na Sevilla.

No comments:

Post a Comment