KIUNGO wa Manchester City, Kevin De Bruyne amekiri kuwa angeweza kubakia Ujerumani kwa msimu mwingine zaidi kama mpenzi wake asingekuwa akitegemea kujifungua. De Bruyne mwenye umri wa miaka 24, alihamia City akitokea Wolfsburg kwa kitita cha paundi milioni 54 majira ya kiangazi mwaka jana ambapo tayari ameshafunga mabao matano na kusaidia mengine nane katika mechi 15 za Ligi Kuu alizocheza. Lakini nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji sasa amebainisha kuwa angeweza kuendelea kubakia Ujerumani kama sio masuala binafsi. Akihojiwa De Bruyne amesema kuzaliwa kwa mwanaye ni jambo kubwa kufanyika katika maisha yake na ndio lilichangia kwa kiasi kikubwa kuhama mapema kuliko alivyotegemea. De Bruyne aliendelea kudai kuwa kama lisingekuwa suala hilo angeendelea kubakia Wolfsburg walau kwa msimu mwingine zaidi.
No comments:
Post a Comment