Monday, May 2, 2016

GUARDIOLA KATIKA KIBARUA KIZITO KESHO.

MENEJA wa Bayern Munich, Pep Guardiola anajua kuwa anatakiwa kuwaziba midomo wakosoaji wake kwa kubadili matokeo na kuhakikisha anapata ushindi katika mchezo wa marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid kesho. Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika kule Vicente Calderon, Bayern walichapwa bao 1-0 ambalo lilifungwa kwa jitihada binafsi za nyota wa Atletico Saul Niguez. Akiwa amewahi kushinda mataji 14 katika kipindi cha miaka minne aliyokuwa Barcelona na sita mpaka sasa katika muda wa miaka aliokaa Bayern, Guardiola ana matumaini ya kuondoka Ujerumani kwa kutwaa taji hilo katika fainali itakayofanyika Mei 28 jijini Milan. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Bayern wamekuwa wakikwama katika hatua ya nusu fainali kwenye michuano hiyo kwa kutolewa na timu za Hispania, mara ya kwanza wakitolewa na Real Madrid na msimu uliopita Barcelona. Kutolewa tena katika hatua hiyo na timu ya Hispania hakutachukuliwa vyema haswa kutokana na uamuzi wa Guardiola alioufanya katika mchezo wa mkondo wa kwanza kumuweka benchi Thomas Muller ambaye ndio mfungaji wa timu hiyo aliyefunga mabao mengi kwa timu hiyo kwenye michuano hiyo. Hata hivyo Bayern wataingia katika mchezo huo wakiwa na rekodi nzuri ya kushinda mechi zao zote tano za michuano hiyo wlaizocheza nyumbani lakini walihitaji muda wa nyongeza kutoka nyuma wakiwa wamefungwa mabao 2-0 na kuichapa Juventus kwa mabao 4-2 katika hatua ya 16 bora.

No comments:

Post a Comment